Revelation of John 14

Mwana-Kondoo Na Wale 144,000

1 aKisha nikatazama na hapo mbele yangu alikuwepo Mwana-Kondoo, akiwa amesimama juu ya Mlima Sayuni. Pamoja naye walikuwa wale 144,000 wenye Jina la Mwana-Kondoo na Jina la Baba yake likiwa limeandikwa kwenye vipaji vya nyuso zao. 2 bNami nikasikia sauti kutoka mbinguni kama sauti ya maji mengi yaendayo kwa kasi na sauti kama ngurumo ya radi. Sauti hiyo niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi wakipiga vinubi vyao. 3 cNao wakaimba wimbo mpya mbele ya hicho kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe wanne wenye uhai na wale wazee. Hakuna mtu yeyote aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao 144,000 waliokuwa wamekombolewa kutoka duniani. 4 dHawa ndio wale ambao hawakujitia unajisi kwa wanawake, kwa kuwa wao ni bikira. Wao humfuata Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamekombolewa kutoka miongoni mwa wanadamu wakawa malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo. 5 eVinywani mwao hapakuonekana uongo, wala hawakuwa na hatia yoyote.

Malaika Watatu

6 fKisha nikamwona malaika mwingine akiruka juu angani, naye alikuwa na Injili ya milele ya kuwatangazia wale waishio duniani, yaani, kwa kila taifa, kabila, lugha na jamaa. 7 gAkasema kwa sauti kubwa, “Mcheni Mungu na kumpa utukufu, kwa maana saa ya hukumu yake imewadia. Mwabuduni yeye aliyeziumba mbingu, dunia, bahari na chemchemi za maji.”

8 hMalaika wa pili akafuata akisema, “Umeanguka! Umeanguka Babeli Mkuu, ule uliyafanya mataifa yote kulewa kwa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake.”

9 iMalaika wa tatu akawafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, “Kama mtu yeyote anamwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa chapa yake kwenye kipaji chake cha uso au kwenye mkono wake, 10 jyeye pia atakunywa mvinyo wa hasira kali ya Mungu ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake pasipo kuchanganywa na maji. Naye atateswa kwa moto uwakao na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele za Mwana-Kondoo. 11 kNao moshi wa mateso yao hupanda juu milele na milele. Hakuna mapumziko, mchana wala usiku, kwa wale wamwabuduo huyo mnyama na sanamu yake, au kwa yeyote anayepokea chapa ya jina lake.” 12 lHapa ndipo penye wito wa subira na uvumilivu wa watakatifu; wale wanaozishika amri za Mungu na kudumu katika uaminifu kwa Isa.

13 mKisha nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika: Wamebarikiwa wafu wafao katika Bwana tangu sasa.”

“Naam,” asema Roho, “watapumzika kutoka taabu zao, kwa kuwa matendo yao yatawafuata.”

Kuvuna Mavuno Ya Dunia

14 nNikatazama, hapo mbele yangu palikuwa na wingu jeupe, na aliyekuwa ameketi juu ya hilo wingu alikuwa “kama Mwana wa Adamu” mwenye taji ya dhahabu kichwani mwake na mundu mkali mkononi mwake. 15 oKisha malaika mwingine akaja kutoka hekaluni naye akamwita kwa sauti kubwa yule aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu akasema, “Chukua mundu wako ukavune kwa kuwa wakati wa mavuno umewadia, kwa maana mavuno ya dunia yamekomaa.” 16Hivyo yule aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu akauzungusha mundu wake duniani, nayo dunia ikavunwa.

17 pMalaika mwingine akatoka katika hekalu lililoko mbinguni, naye pia alikuwa na mundu mkali. 18 qKisha malaika mwingine, aliyekuwa na mamlaka juu ya moto, akatoka kwenye madhabahu, naye akamwita yule malaika mwenye mundu mkali kwa sauti kubwa, akisema, “Chukua mundu wako mkali ukakusanye vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva.” 19 rHivyo yule malaika akauzungusha mundu wake duniani na kukusanya zabibu za dunia na kuzitupa kwenye shinikizo kubwa la ghadhabu ya Mungu. 20 sLile shinikizo likakanyagwa nje ya mji, nayo damu ikatiririka kama mafuriko kutoka hilo shinikizo kufikia kimo cha hatamu za farasi,
Kimo cha hatamu za farasi ni kama mita moja na nusu.
kwa umbali wa maili 200.
Maili 200 ni sawa na kilomita 320.
Copyright information for SwhKC